Friday, April 1, 2016

Balozi Seif ahimiza uadilifu kufanikisha malengo


MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewataka watendaji wa taasisi za umma nchini kuwa makini zaidi katika kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha kwenye taasisi.
Alitahadharisha kwamba kipindi hiki hali ya fedha si nzuri kutokana na mambo mengi yaliyofanywa katika kipindi kifupi kilichopita ikiwemo suala la uchaguzi mkuu ambalo limelazimika kutumia fedha nyingi, zaidi baada ya kujitokeza wa uchaguzi wa marudio.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wawakilishi wa watendaji wa taasisi zilizo chini ya Ofisi yake walipompokea rasmi kuingia ofisini kwake na kuanza kazi mara baada ya kuteuliwa tena na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohammed Shein kushika wadhifa huo katika kipindi kingine cha miaka mitano ijayo.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuendesha taasisi zake za Umma kwa kutumia fedha inazokusanya kupitia vianzio vyake mbalimbali chini ya usimamizi wa watendaji watakaoonesha uadilifu kwenye usimamizi huo.
Ametaka taasisi za fedha ikiwemo bodi ya mapato na mamlaka ya kodi nchini TRA kuwa wabunifu zaidi katika kutafuta fedha katika vyanzo vipya kwa lengo la kuona Serikali inatekeleza malengo yake vizuri ili kupambana na baadhi ya washiriki wa maendeleo ambao wametishia kusitisha misaada yao kwa kisingizio cha uchaguzi wa marudio.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea kuchukiwa kwake na baadhi ya watendaji wa Umma wenye tabia mbaya ya kuwekeana chuki katika utekelezaji wa majukumu yao yanayowakabili ya kila siku, hatua ambayo husababisha kushuka kwa utendaji na uzalishaji sehemu za kazi.
Balozi Seif pia aliwapongeza na kuwashukuru viongozi pamoja na watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake kwa kazi kubwa waliyoifanya iliyomuwezesha kutekeleza majukumu yake ya ufanisi mkubwa ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.
Mapema Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Ahmad Kassim kwa niaba ya watendaji wa ofisi hiyo amempongeza Balozi Seif kwa kuteuliwa tena kushika wadhifa huo hatua ambayo inaonesha uwezo wake katika kusimamia shughuli za serikali.

No comments:

Post a Comment