Yanga yaitega Al Ahly
KOCHA wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema ameandaa mbinu tatu kuiangamiza Al Ahly ya Misri kwa ushindi wa kishindo zitakapokutana katika mchezo wa kwanza Raundi ya Pili Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mchezo huo utafanyika Aprili 9, mwaka huu, Uwanja wa Taifa uliopo Wilaya ya Temeke Dar es Salaam, kisha zitarudiana wiki mbili baadaye mjini Cairo, Misri.
Akizungumza na gazeti hili, Pluijm alisema sababu ya kuandaa mikakati hiyo ni kutokana na ubora na uzoefu waliokuwa nao Al Ahly ambao kwa sasa wanafundishwa na Mholanzi mwenzake Martin Jol, aliyewahi kuzifundisha timu za Tottenham na Fulham zinazoshiriki Ligi Kuu ya England.
“Huu ni mchezo mkubwa na tunakutana na timu yenye rekodi nzuri Afrika na wachezaji na kocha mwenye uzoefu mkubwa, hivyo ni vyema tukajipanga kwa kuwa na mbinu nyingi za kivita,” alisema.
Alisema anachotaka ni kuona timu yake inapata ushindi wa mabao yasiyopungua matatu nyumbani ili waweze kuwa na kazi nyepesi ya kulinda ushindi wao mchezo wa marudiano.
Alisema katika kuhakikisha mipango yake inafanikiwa anachokifanya kwa sasa ni kuliandaa jeshi lake hasa kikosi kitakachoanza siku hiyo ili kicheze na kutimiza majukumu atakayowaelekeza. “Nawajua Al Ahly, ni mara ya pili sasa tunaenda kucheza nao siyo timu mbaya, lakini hawatishi kama inavyozungumzwa mitaani.
“Najua mbinu za kocha wao wa sasa ni rafiki yangu, Mholanzi mwenzangu ingawa yeye hazijui za kwangu kwa hiyo naamini tuna nafasi nzuri ya kuweka rekodi ya kuwatoa na kucheza hatua ya makundi mwaka huu,” alisema Pluijm.
No comments:
Post a Comment