Wednesday, March 23, 2016

Waziri Nape awaahidi neema muziki wa dansi



WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ameahidi kupambana na kila aina ya udhalimu unaoikabili tasnia ya muziki wa dansi nchini.
Nape alitoa ahadi hiyo katika mkutano wake na wanamuziki wa dansi uliofanyika juzi katika ukumbi wa Vijana uliopo Kinondoni, Dar es Salaam.
Alisema kutokana na mchango mkubwa wa muziki wa dansi katika nchi hii unastahili heshima na wanamuziki wake kuwa na maendeleo makubwa.
Aliongeza kuwa tofauti na inavyotarajiwa, muziki huo umekuwa ni kama wa kawaida huku wasanii wake kila kukicha wakiwa na malalamiko ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi haraka.
Nape alisema hayo baada ya kupokea malalamiko kadhaa kutoka kwa wanamuziki wa muziki huo.
Akiendelea kujibu kero kadhaa, alisema kuwa kodi, uharamia, kudhulumiwa pamoja na kutopewa kipaumbele katika vituo vya redio ni moja ya changamoto kubwa za muziki huo.
Akizungumzia kuhusu kodi, alisema kwa kuwa serikali inahitaji mapato kutoka katika kila sekta, hawezi kuwasaidia kuondoa kodi ya kuingiza vyombo vya muziki ila anaweza kusaidia kupatikana urahisi wake. Pia akizungumzia kutopewa kipaumbele kwa nyimbo za dansi katika redio, aliwataka wasanii hao kumuachia suala hilo.
Pia aliongeza kuwa: “Nimeamua kuja kuwasikiliza mwenyewe kama Waziri wenu na ninataka kuwahakikishia kuwa harakati za Rais John Magufuli za kuwasaidia zitafanikiwa tu, na kazi ndio inaanza,” alisema.

No comments:

Post a Comment