Wednesday, February 24, 2016


Mmoja wa waathirika wa ndoa za utotoni akifanya majukumu yake ya nyumbani.

 
KATIKA tamaduni nyingi za kitanzania, wasichana wanadhaniwa kuwa tayari kuolewa wanapovunja ungo.
Mara nyingi ndoa inaonekana kama njia ya kuwalinda dhidi ya ngono na mimba za kabla ya ndoa ambazo zinashusha heshima ya familia na kuweza kushusha kiasi cha mahari ambayo familia itapokea. Jamii katika makabila kadhaa wanaona kumuoza mtoto mapema ni namna ya kupata usalama wa kifedha kwao na kwa mabinti zao na kubwa kupunguza mzigo kwa familia.
Utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) umebaini kuwa ndoto hizo hazina ukweli wowote kwani badala ya kuwa faraja, ndoa za utotoni zimeongeza utegemezi katika familia na jamii husika. Hali hii inatokana na kuwa wengi wanaoolewa wanakuwa hawana elimu ya kutosha kuweza kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na wengine hulazimika kuishi katika mazingira ya familia aliyoolewa kutokana na mume wenyewe kutokuwa na uwezo wa kujitegemea anapoanzisha familia mpya.
Wengi wanaoolewa katika ndoa za utotoni ni wale waliofeli mtihani wa kumaliza elimu ya msingi. Wengi wa watoto hawa hutoka familia masikini zenye vipato vya chini. Wasichana hao elimu inakuwa haijawasaidia na wanarudi nyumbani kuishi na wazazi wao katika hali zao za umasikini, kwa sababu hakuna hata elimu ya ujasiriamali inayofundishwa ili kuwaandaa watoto hawa kuwa wajasiriamali.
Pia hawana elimu ya uraia itakayowaandaa kukabiliana na changamoto za maisha pindi warudipo nyumbani, wala hakuna chochote wanachokuwa wameandaliwa watakapofeli mtihani kwamba wanaweza kukifanya ili kujimudu kimaisha, wanakuwa hawana mtaji wa namna yoyote ile; si maarifa wala fedha. Tafiti zinaonesha kuwa asilimia 39 ya watoto wa kike wenye elimu ya msingi wameolewa katika umri usiotarajiwa chini ya miaka 18 wakati wale wenye elimu ya kutosha wa mjini wameolewa baada ya kufikisha miaka 18.
Mwanaharakati katika kijiji cha Kidoka wilayani Chemba, Mwanahamisi Ngede anasema kati ya watoto sita walioolewa mwaka juzi mara baada ya kumaliza elimu ya msingi wakiwa katika umri mdogo usiozidi miaka 14, wanne wanaishi kwenye familia walizoolewa na wawili wamepelekwa nje ya eneo hilo. Lakini wengi walioolewa wanalazimika kusaidiwa katika kuendesha maisha na kulea watoto kutokana watoto kuwa na watoto wenzao au kuwa na umri ambao hauwezi kufanya binti huyo kusimamia na kuendesha maisha ya familia yake.
Ndoa za utotoni zinazosababisha mimba za utotoni na kupelekea zaidi umasikini. Emma Chaloo ambaye kijana wake wa miaka 24 amefunga ndoa na binti wa miaka 14 na tayari wamepata mtoto mmoja wa kiume, anasema kumpata mkwe huyo kumeongeza mzigo katika familia yake.
“ Yeye na mumewe wanakaa pale (anaonesha kijumba kilicho pembeni mwa nyumba ya wazazi wao, muda wote anashinda hapa kwangu, anafua hapa na kufanya shughuli zake hapa. “ Hata akikwama chumvi, au wakikosa chakula wanakuja hapa. Kwangu amekuwa ni mtoto mwingine wa familia ambaye natakiwa kumtunza sambamba na mjuu aliyemzaa,” anabainisha Chaloo.
Asha ambaye ni mama wa nyumbani akiwa na jukumu kubwa la kumlea mtoto wake, anasema anategemea kila kitu kwa mume wake na familia ya mumewe. “ Kwa sasa sina kazi yoyote ya kuniingizia kipato, ninategemea kile anachotafuta mume wangu, nikikwama naenda kwa wakwe, nako hali ikiwa ngumu naenda nyumbani kwetu. “ Nikipata mtaji naweza kufanya biashara ambazo najua zitaniongezea kipato badala ya kumtegemea mume pekee, anabainisha Asha.”
Mbali na utegemezi wa kiuchumi, lakini pia wamekuwa na utegemezi wa mawazo hivyo maamuzi ya wasichana hawa hutegemea watu wengine. Pia hata maamuzi ya msingi kwa binti yanapangwa na wazazi wa ukweni kama uamuzi wa kufuata njia ya uzazi wa mpango na mambo mengine ambayo mke na mume ndio waliotakiwa kukubaliana kabla ya kutekeleza uamuzi huo.
Katika kuonesha utegemezi huo, anamuuliza mwandishi wa makala haya njia nzuri ya uzazi wa mpango ili amnusuru binti huyo kupata ujauzito mwingine kabla ya mtoto wa kwanza kukua. “ Ni lazima nimsaidie mkwe wangu, nikimuacha basi atapata mimba nyingine kabla ya mtoto wa kwanza kukua, maana hajui chochote. Sitaki abebe mimba nyingine nataka apumzike kwanza,” anasema Chaloo.
Wakati mama mkwe akionesha hofu ya mkwewe kuwa na uwezekano wa kupata ujauzito mwingine kabla ya mtoto kukua, Asha haoneshi kuwa na mawazo ya kufuata uzazi wa mpango. “Mimi sijui chochote, nitafuata kile mama mkwe atakavyoniambia. Kama atanipeleka hospitalini kwa ajili ya kupata utaalamu wa uzazi wa mpango nitafanya hivyo,” anasema Asha wa kijiji cha Kidoka wilayani Chemba.
Ofisa wa Taasisi ya Dodoma Inter Africa Commettee (DIAC), Daniel Msangya anasema taasisi yake imekuwa ikiwasaidia wale waliokumbwa na matatizo ya kuolewa katika umri mdogo ili waweze kujikwamua kimaisha na kuinua kipato katika familia zao. Anatolea mfano katika kijiji cha Faraqwa wilayani Chemba ambako tayari wameshatambua wasichana 20 waliolewa wakiwa na umri mdogo ambao wanafanyiwa utaratibu wa kusaidia.
“Hatuwezi kuwaondoa kwenye ndoa zao, tunacholenga kufanya ni kuwawezesha kwa kuwapa elimu na kuwajengea uwezo wa kutambua mazingira na kuwapa stadi za maisha kwa kutoa elimu ya afya ya uzazi, ujasiriamali na uendeshaji wa vikundi vya kuweka na kukopa. “ Tunajua kwa kufanya hivi, tutaondoa tatizo la utegemezi kwa wasichana hao na kupunguza mzigo wa maisha katika familia zao,” anasema.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii katika Wilaya ya Chemba, Flora Shija anasema pamoja na kutokuwa na tukio la ndoa za utotoni, idara yake imejipanga kulifuatilia hilo kwa makini na kuangalia namna ya kuwasaidia. “ Tutaenda vijijini kuangalia, kama tutawakuta wako katika ndoa zao, tutakachoweza fanya ni kusaidia kupata mikopo ya kufanya biashara ndogo ndogo kama ambavyo sasa tunafanya kuinua vikundi vya wanawake,” anasema Shija.

No comments:

Post a Comment