Monday, February 29, 2016

Yanga yanogewa Pemba


VINARA wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, Yanga wamerejea kisiwani Pemba kusaka makali ya kuiua Azam FC katika mchezo wao wa mwishoni mwa wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga imerejea huko ikiwa ni kumbukumbu nzuri ya kuweka kambi kisiwani huko na kuja kuiadhibu Simba kwa mabao 2-0 katika mchezo mwingine wa ligi kuu uliofanyika Jumamosi ya Februari 20, mwaka huu.
Hayo yalithibitishwa jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, akisema kikosi cha wachezaji wote wa klabu hiyo bingwa nchini kitakuwa Pemba kujinoa katika mazingira tulivu ili kujiandaa na mchezo wao muhimu dhidi ya Azam.
Mpaka sasa, timu hizo zinakabana koo kileleni, kila moja ikiwa na pointi 46 baada ya kushuka dimbani mara 19, lakini Yanga ikiongozwa kwa kuwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Mchezo baina ya timu hizo umebeba taswira halisi ya nani atajiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa msimu huu na timu zote zimewekeza katika maandalizi mazuri ndani na nje ya Uwanja.
Azam, kabla ya mchezo huo leo inachuana na Panone FC ya Moshi katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litakalotoa mwakilishi wa nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) mwaka kesho.
Akizungumzia kambi ya Pemba, Muro alisema Yanga inayonolewa na Mholanzi Hans Pluijm ilitarajiwa kutua jana mchana kwa ndege maalumu ya kukodi.
“Ni kweli tunakwenda kuweka kambi Zanzibar kwa ndege maalumu ya kukodi, kujiandaa na mchezo wetu ujao lengo ni kukaa katika mazingira tulivu na kuhakikisha tunashinda,” alisema.
Mbali ya kuwa na kumbukumbu ya kuitungua Simba, Yanga pia imeanza vyema michezo ya kuwania ubingwa wa Afrika, baada ya mwishoni mwa wiki kuing’oa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0.
Lakini kocha Pluijm amesema pamoja na kufanya vizuri kwa kikosi chake, bado ana kazi ya kukiandaa kikosi chake kiweze kupata ushindi dhidi ya Azam.
Pamoja na kufungana kwa pointi na idadi ya michezo, Yanga na Azam zina mambo yanayofanana, mathalani, zote zimepoteza mechi moja moja, mbabe wao akiwa Coastal Union ya Tanga. Aidha, hivi karibuni zote zilitoka sare dhidi ya Prisons ya Mbeya.

No comments:

Post a Comment