Sunday, February 28, 2016

Vyuo vya ualimu vyamwagiwa fedha


SERIKALI imetenga Sh bilioni 1.65 kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwenye vyuo vya ualimu nchini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema juzi kwamba fedha hizo zinapaswa zitumike kulipia posho za kujikimu, nauli na ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia.
Alitoa taarifa hiyo juzi wakati akizungumza na walimu na watumishi wa sekta ya elimu kutoka wilaya zote za Mkoa wa Mtwara uliofanyika mjini hapa.
“Serikali inatambua umuhimu wa mafunzo kwa vitendo katika vyuo vya ualimu ni kwa sababu hiyo mwezi huu wa Februari tumetoa Sh bilioni 1.65 kwa vyuo vya ualimu 35 vya umma nchini ili kuwezesha wakufunzi na walimu wanafunzi kushiriki kikamilifu mafunzo kwa vitendo ,” alisema huku akishangiliwa.
Awali, akizungumza na wakazi wa Mtwara kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mashujaa, Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kuimarisha elimu na akaonya wote wanaofikiria kuwaharibia elimu watoto wa kike.
“Tunataka watoto wa kike wasome wa Kitanzania wasome hadi elimu ya juu waje wawe watumishi wa umma hapo baadaye. Kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake tukikumbuka kaulimbiu ya Mama Salma Kikwete ya kwamba ‘Mtoto wa Mwenzio ni wako,” alisema.
“Yeyote atakayemharibia mtoto wa kike masomo kwa kumrubuni na chips au pipi ajiandae kwenda Lilungu, (gereza la mkoa wa Mtwara)”, alisema.

No comments:

Post a Comment