KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imesema imeridhishwa na maandalizi ya uchaguzi wa marudio Zanzibar na kutaka ifahamike kuwa siasa za Zanzibar hazitawaliwi na vyama viwili.
Hayo yalielezwa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kikao maalumu cha Kamati Kuu kilichofanyika mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete.
Akijibu swali aliloulizwa kuwa chama hicho kinajisikiaje kushiriki uchaguzi ambao umesusiwa na Chama cha Wananchi (CUF), Nape alisema siasa za Zanzibar hazitawaliwi na vyama viwili, bali kuna vyama vingine vinavyoendesha siasa visiwani humo.
“Siasa ya Zanzibar haitawili na hivi vyama viwili bali kuna vyama vingine vingi tu, kwa hiyo anayesusa acha asuse sisi wengine tunaendelea,” alisema Nape. Alisema kamati hiyo imepokea taarifa ya maandalizi ya uchaguzi huo na imewatakia kila la kheri Wazanzibari ili wamalize uchaguzi huo salama na kuwapata viongozi waliowakusudia.
Aidha, alisema kuhusu makamishna wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kujitokeza na kupinga maamuzi ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jecha Salum Jecha kwa madai amekuwa akijiamulia mambo bila kuwashirikisha, Nape alitaka watu kuheshimu sheria.
Wakati huo huo, Nape amesema Kamati Kuu ya chama hicho imetoa pole kwa Jeshi la Polisi nchini kutokana na vifo vya asakri polisi watatu vilivyotokea Februari 6, mjini Singida kutokana na ajali.
No comments:
Post a Comment